Barua ya Wazi Kwa Waziri Anthony Blinken Anapoizuru Rwanda na Kongo

Mheshimiwa Blinken,

Ninakuandikia kukupongeza kwa juhudi zako kusafiri kwenda nchini Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wiki ijayo katika kutafuta amani Mashariki mwa Afrika.

Marekani imekuwa mshirika wa karibu na wa muda mrefu wa utawala wa raisi Kagame tangu aingie madarakani mnamo 1994, baada ya vita vibaya vilivyosababisha mauaji ya kimbari.

Kundi la wataalamu kutoka Umoja wa Mataifa limethibitisha kile ambacho kimekuwa siri kwa wana Afrika Masharik na mataifa mengine kwamba, tangu Novemba 2021, Rwanda imekuwa ikiendesha mashambulizi ya kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kutumia mgongo wa waasi, M23. Kama ilivyokuwa mwaka 2012 amabapo waasi wa M23 na washirika wake kutoka Rwanda walivyoushika mji wa Goma, sasa wameshikilia miji na vijiji mashariki mwa Kongo DRC.

Tangu kuingia kwake madarakani nchini Rwanda mwaka 1994, baada ya vita vibaya vya kiraia vilivyopelekea mauaji ya kimbari, utawala wa Kagame umekuwa tishio endelevu katika uchumi wa Kongo pamoja na mipaka yake. Kuanzia Vita vya Kwanza vya Kongo (1996-1997), Vita vya Pili vya Kongo (1998), mfululizo wa vita vinavyoendeshwa kwa mgongo wa waasi, pamoja na uvamizi huu wa sasa —mpango wa Rwanda ni kuidhoofisha na kuiendesha Kongo, pamoja na kujifanya mkombozi wa migogoro katika eneo hilo.

Kila mara Rwanda inapovamia Kongo; kwanza hukana kuhusu iuvamizi huo, kisha hudai kwamba ni kwa lengo la kufuatilia watu wenye nia ya kuleta mauaji ya kimbari, vilevile hujifanya kuwa ni balozi na kinara wa kutetea haki za watu wa kabila la Watusi (Banyamulenga). Inakadiriwa kuwa zaidi ya Wakongomani milioni 5.4 na mamia ya Wahutu wamefariki kutokana na vita hivi endelevu vilivyoanzishwa na kuendeshwa na utawala wa Kigali. Ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN DRC Mapping Report 2018) inaonyesha jeshi la Rwanda likijihusisha na vitendo vya dhuluma dhidi ya binadamu, uhalifu wa kivita, pamoja na vitendo vinavyoashiria mauaji ya halaiki dhidi ya Wahutu na Wakongomani (OHCHR | DRC: Mapping human rights violations 1993-2003).

Utawala wa Raisi Kagame haujawahi kuwajibishwa kwa maovu haya yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wewe ni mwanafunzi mzuri wa historia na vilevile mbobevu katika uhusiano wa kimataifa. Hivyo unafahamu vyema kwamba sera ya ndani ya taifa hupelekea namna gani taifa hilo litahusiana na mataifa mengine. Utawala wa mabavu ndani ya nchi hujidhihirisha kwa kuonyesha vurugu kwa majirani. Uwezekano wa kuwepo maridhiano ya amani na usalama baina ya Rwanda na Kongo ni matuamaini matupu endapo mzizi wa ubabe, mauaji ya halaiki, na mipango ya vita inayoandaliwa nchini Rwanda haitapatiwa ufumbuzi —yaani kukomeshwa.

Chini ya awamu yako ya Uongozi, Idara ya Serikali ya Marekani katika ripoti yake ya mwaka 2021, imezungumzia hofu wanayolazimika kuivumilia Wanyarwanda kutoka kwa polisi huku wakinyimwa njia za amani za kutaka mabadiliko.(https://www.state.gov/reports/2021-country-reports-on-human-rightspractices/rwanda)

Taarifa za kuaminika kuhusu maswala ya haki za binadamu zinaonyesha; uvunjifu wa sheria au mauaji ya kiholela yanayofanywa na serikali; kupotezwa kwa watu na serikali; kuteswa, ukatili pamoja na adhabu zisizo za kibinadamu zilizofanywa na serikali; hali mbaya ya magereza inayotishia uhai; kukamatwa na kuzuiliwa bila uataratibu; kuwepo kwa wafungwa wa kisiasa au waliowekwa kizuizini; visasi vya kisiasa dhidi ya watu waishio nje ya Rwanda, ikiwemo mauaji, kutekwa, na kufanyiwa vurugu; kuingiliwa bila utaratibu juu ya uhuru wa faragha; vizuizi vya nguvu juu ya uhuru wa maoni na habari, ikiwemo vitisho na vurugu dhidi ya waandishi wa habari, kufungiwa kwa maudhui; vizuizi vikali juu ya uhuru wa mtandao; kuvamiwa kwa mikutano ya amani na kubinywa uhuru wa kuandamana, ikiwemo sheria kandamizi juu ya mashirika, uwezeshwaji kifedha, na shughuli za mashirika na asasi za kiraia; vizuizi vikali juu ya ushiriki kisiasa; pamoja na vizuizi vya serikali au pengine unyanyasaji kwa mashirika ya haki za biandamu ya ndani na yale ya kimataifa.

Utawala wa Kagame umekuwa kwenye vita visivyoisha na Kongo kwa sababu, kwa ndani, utawala huu una vita endelevu na wananchi wake. Kwakuwa utawala wa Kigali haujawahi kuwajibishwa, Kagame amekuwa na ujasiri wa kuanzisha vita nyingine nchini Kongo na kutaka kuongeza muda wake wa kusalia madarakani kwa miaka mingine 20.

Alama kuu ya Kagame ni utawala usiojali, usiowajibika, uchokozi kwa nchi jirani, njama za mauaji halaiki, udanganyifu na kutokuheshimu maisha ya watu nchini Rwanda na Kongo. Tangu kipindi cha vita baridi, hakujawahi kutokea tishio la usalama na ustahimilivu Afrika Mashariki na Kati kama hili, lenye kuleta madhara makubwa ya kiutu; upotevu wa maisha, na kuvuruga mifumo ya kijamii na uchumi.

Tawala mfululizo za Marekani kuanzia Raisi Clinton, Bush, Obama, na Trump zimeupa ruksa utawala wa Kagame kufanya yanayofanyika kwa sababu za kimkakati pamoja na ile hali ya Marekani kujihisi hatia juu ya mauaji ya kimbari.
Maoni ya Wanyarwanda, Wakongomani, na Waafrika wengi ni kwamba huduma za kisiasa, diplomasia na kifedha kutoka Marekani ndiyo zinafanya utawala wa Kagame kuendelea kufanya vitendo vya uavamizi na uchokozi kwa nchi jirani.

Mtazamo wa walipa kodi wa Marekani unaona ni upotevu, si haki, na si utu kutumia pesa zao kwenye utawala usiojali uhuru wa wananchi wake na kuendesha vita viletavyo uharibifu dhidi ya nchi jirani.

Kuna mambo machache nigependa kukushirikisha kuhusu Kagame na jinsi mambo yafanyikavyo ndani ya utawala wake. Ninaufahamu vyema utawala wa Kagame kwani niliwahi kuwa miongoni mwa viongozi wa juu kipindi cha kuanzishwa kwa utawala huo mwaka 1994. Nilianza kwa kuwa katibu mkuu wa chama pekee cha RPF, nikaja kuwa Balozi wa Rwanda nchini Marekani, na baadaye kuwa Msaidizi wa ngazi ya juu wa Kagame.

Kwanza kabisa, usiweke matumaini makubwa unapozungumza na wapatanishi wadanganyifu wa Rwanda. Hakuna suluhu ya haraka kwenye matatizo haya sugu ya Afrika Mashariki. Ingawa unaweza kufikia maridhiano kadhaa na Raisi Kagame, lakini hutoweza kubadili tabiya yake anayoifanya kwa wananchi wa Rwanda na Kongo.

Kagame anategemea na anastawi katika utawala wa kiimla, utawala wa mabavu, vurugu, hofu, kutengeneza vita, njama, kutokujali, pamoja na kujikita katika mipango hatarishi. Kagame huvunja ahadi mara tu azitoapo. Amekuwa mlevi wa mtindo huu wa utawala ambao umemsaidia vyema kwa miaka 30 sasa. Hayuko tayari kutelekeza mtindo huu wa utawala pamoja na kuwepo viashiria kwamba utawala wa aina hii uko mbioni kuanguka.

Hivyo kuwa mkweli unapozungumza na Kagame. Mkumbushe kuwa eneo lenye migogoro kamwe halina tija, ni hatari na haliwezi kuleta maendele endelevu. Zaidi huleta machafuko, vurugu na fujo za kudumu. Mpatie ujumbe bila kupepesa kwamba utawala wake unatakiwa kuachana na ukiukaji haki za binadamu, awaachie mateka wote na wafungwa wa kisiasa, mashirika na asasi za kiraia kuweza kufanya shughuli zake bila kusumbuliwa. Msisitize kwamba ushirikiano baina ya Marekani na Rwanda umejikita katika misingi ya uwajibikaji, haki za binadamu, utawala wa sheria pamoja na demokrasia.

Jambo la pili, bila kuficha maneno, muweke wazi Raisi Kagame kwamba Marekani haitasita kutumia mchango wako kidiplomasia, siasa na kifedha kuondoa utawala wa Kagame uliokubuhu kwa udhalimu dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Iwajibishe Rwanda kwa maovu iliyoyafanya, pamoja na uporaji mali ghafi inaoendelea kuufanya nchini Kongo.

Wanyarwanda, Wakongomani na wana Afrika Mashariki wanahitaji haki. Si utawala dhalimu wa kidikteta. Ni matakwa ya wananchi, ambayo mojawapo ni uhuru, ndiyo serikali ya Marekani inatakiwa kuyazingatia.

Vilevile, sera na mikakati ya Marekani kuhusu Rwanda inatakiwa kuachana na kutafuta faida za muda mfupi, mikakati finyu ya ukanda, na kuacha kujiona wenye hatia juu ya mauaji ya kimbari. Mambo haya ndiyo yamepelekea mwenendo wa sera ya Marekani nchini Rwanda kwa muda mrefu. Kuachana na mambo haya kutaleta tija katika matakwa ya Marekani. Kutaleta uwajibikkaji, uhuru, amani, usalama pamoja na ustawi wa jamii nchini Rwanda, Kongo DRC na Afrika Mashariki.

Ninakutakia safari njema nchini Rwanda na yenye kuzaa matunda.

Wako katika maendeleo.

Dr. Theogene Rudasingwa
Katibu, Rwanda Truth Commission
Mwenyekiti, Harakati za Ukombozi Rwanda
Washington DC
USA
Agosti 6, 2022